Shabana Iko Imara, Beki Alvin Ochieng Aeleza Imani ya Kuepuka Kushushwa Ngazi.

Beki wa kulia wa Kilabu ya Shabana FC, Alvin Ochieng, ametoa matumaini ya uhakika kwamba timu yake haitashuka daraja msimu huu katika Ligi Kuu ya FKF. Ochieng ameeleza kuwa ili kuthibitisha nafasi yao kwa msimu ujao, wanahitaji angalau ushindi katika mechi tatu zinazofuata.

Shabana FC imeonyesha mwendo imara katika mechi zao nne zilizopita, wakipata alama 10 kati ya 12 zilizopo. Mafanikio yao yalifika kileleni mwishoni mwa wiki iliyopita waliposhinda dhidi ya Sofapaka kwa bao 1-0.

Ushindi huo uliwaondolea wasiwasi wa kushuka daraja na kuwapeleka kwenye nafasi ya 15 kwenye msimamo wakiwa na alama 28, wakizidiwa alama mbili tu na Talanta FC.

Ochieng, ambaye yuko Shabana kwa mkopo kutoka Gor Mahia, amesisitiza uwezekano wa timu yao kujikwamua. Beki huyo anaamini kwamba ushindi katika mechi tatu zijazo utakuwa wa kutosha kuwawezesha Shabana kuepuka kushuka daraja msimu huu. Shabana watakua na kibarua kigumu wikendi hii, watakapovunjana miguu na viongozi wa ligi Gor Mahia kwenye uwanja wa Mamboleo Mjini Kisumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *