Mbappe Atangaza Kuwa Ataondoka PSG Mwishoni mwa Msimu Huu.

Mbappe Kuondoka PSG

Mshambulizi matata wa kilabu ya Paris Saint-Germain (PSG), Kylian Mbappe, amethibitisha kuondoka kwake kutoka klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Kupitia video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mbappe, mwenye umri wa miaka 25, amethibitisha uvumi uliokuwa ukienea kwa muda mrefu. Mfaransa huyo ambaye amekuwa PSG tangu mwaka 2018, amecheza mechi 306, akifunga mabao 255 na kutoa assisti 108.

Mbappe, ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2018, ameiongoza PSG kushinda mataji sita ya ligi, mataji matatu ya Kombe la French Cup, mataji mawili ya Kombe la ligi, na mataji manne ya French Super Cup.

Katika tangazo lake la kuondoka, Mbappe amethibitisha kwamba mechi dhidi ya Toulouse itakuwa ya mwisho kwake ugani Parc des Princes akiwa na jezi ya PSG. Amewashukuru wachezaji, viongozi wa klabu, na makocha wote aliowafahamu katika kipindi chake PSG. Pia, ameeleza nia yake ya kucheza nje ya Ufaransa.

Inatarajiwa kwamba Real Madrid itakamilisha uhamisho wa mfaransa huyo, baada ya kuonyesha nia ya kumsajili kwa muda mrefu. Mbappe alikuwa na hamu ya kushinda Ligi ya Mabingwa na PSG, baada ya kuifikisha timu hiyo kwenye fainali mwaka wa 2020, lakini ikashindwa na Bayern Munich.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *