Odada Ajiunga na Kambi ya Stars kwa Michuano ya Kufuzu Kombe la Dunia 2026

Richard Odada, kiungo wa kimataifa wa Kenya anayekipiga katika ligi ya Denmark, amejiunga na kambi ya timu ya taifa ya Harambee Stars inayojiandaa kwa michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast na Burundi.

Awali, Odada alitarajiwa kujiunga na kikosi hicho nchini Malawi, ambapo mechi hizo zitachezwa, lakini taarifa zinaeleza kwamba tayari amewasili na yuko pamoja na wenzake kwenye kambi yao humu nchini.

Nahodha wa Harambee Stars, Michael Olunga, pamoja na beki wa kulia, Daniel Anyembe, wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo nchini Malawi kwa maandalizi ya mwisho. Kenya imeratibiwa kucheza dhidi ya Burundi tarehe 7 mwezi ujao nchini Malawi saa kumi alasiri, kabla ya kukutana na Ivory Coast siku nne baadaye.

Mechi hizi mbili zilipangwa kufanyika nchini Kenya, lakini sasa zitachezwa nchini Malawi kutokana na ukosefu wa viwanja vinavyofaa kwa michuano hiyo. Viwanja vya Kasarani na Nyayo, ambavyo kwa kawaida hutumika kwa mechi hizi, vimefungwa kwa ajili ya ukarabati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *