Kilabu ya Arsenal ilizidisha matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Premier League nchini Uingereza baada ya kupata ushindi wa muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Manchester United katika uga wa Old Trafford siku ya Jumapili. Ushindi huo uliwaweka kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 86, wakiwa mbele kwa alama moja tu dhidi ya Manchester City, ambao bado wana mechi moja mkononi dhidi ya Tottenham Hotspur siku ya Jumanne.
Bao la pekee la Arsenal lilipatikana katika dakika ya 20 kupitia mchezaji Leandro Trossard, aliyeunganisha krosi safi kutoka kwa Kai Havertz. Kikosi cha wana Arsenal kilionyesha udhibiti wa mchezo kwa kiasi kikubwa, huku Manchester United wakionekana kutokuwa na makali katika mashambulizi yao. Ushindi huo ulikuwa ni wa kwanza kwa Arsenal kwenye mechi za ligi katika uwanja wa Old Trafford baada ya miaka 18.
🎶 One-nil to The Arsenal 🎶
Relive today’s 1-0 victory over Manchester United all over again 👇 pic.twitter.com/mVECUZHlfm
— Arsenal (@Arsenal) May 12, 2024
Manchester United, ambao wamekumbwa na majeraha, walilazimika kutegemea wachezaji chipukizi kumaliza mchezo huo, licha ya habari za awali kuashiria kuwa wachezaji kama Marcus Rashford na nahodha Bruno Fernandes walikuwa katika hali nzuri kwa mechi hiyo.
Kufuatia ushindi huo, Arsenal sasa wanahitaji kushinda mchuano wao wa mwisho wa msimu na kuwa na matumaini kwamba Manchester City watapoteza mchezo wao dhidi ya Tottenham au dhidi ya West Ham siku ya mwisho ya msimu, ili (Arsenal) waweze kutwaa ubingwa.