Junior Starlets Waandikisha Historia kwa Kufuzu Kombe la Dunia.

Junior Starlets

Kikosi cha Taifa cha wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 Junior Starlets kimeingia kwenye historia kwa kuwa timu ya kwanza kutoka Kenya kushiriki kwenye Kombe la Dunia la U-17.

Hii ni baada ya ya kusajili ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burundi, katika mechi ya kufuzu iliyoandaliwa jumapili katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex, Jijini Nairobi. Kikosi cha Kenya kilikamilisha mechi za kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0 dhidi ya Burundi baada ya ushindi wa maba0 3-0 katika mkondo wa kwanza.

Mabao ya Marion Serenge na Valerie Nekesa yalitosha kumaliza matumaini ya Burundi ya kufuzu. Serenge alifunga bao la kwanza kabla ya Nekesa kuongeza la pili, yote katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Kikosi hiki, kinachonolewa na kocha Mildred Cheche, kimejipatia nafasi ya kuwa miongoni mwa mataifa matatu kutoka Afrika yatakayoshiriki kwenye Kombe la Dunia la U-17, litakalofanyika mwezi Oktoba mwaka huu huko Jamhuri ya Dominika.

Kufuatia mafanikio yao, Junior Starlets walitunukiwa zawadi ya shilingi milioni 10 na wizara ya michezo. Fedha hizo zitashuhudia wachezaji wote wakijipatia shilingi laki tatu kila mmoja. Kocha Cheche sasa anajiandaa kwa kibarua kikubwa dhidi ya wapinzani wengine 15 katika mashindano hayo ya dunia. Mashabiki wa humu nchini wanatarajia kuona jinsi starlets vijana watapeperusha bendera ya Kenya kwenye mashindano hayo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *