Leverkusen Wavunja Rekodi ya Bara Ulaya na Kutinga Fainali ya Kombe la Europa.

Bayen Leverkusen

Mabingwa wa ligi ya Bundesliga, Bayern Leverkusen, walivunja rekodi ya bara Ulaya iliyodumu kwa zaidi ya miaka 59, baada ya kutopoteza katika michuano 49 mfululizo. Leverkusen waliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu baada ya kutoka nyuma mabao 2-0 dhidi ya Roma na kutinga fainali ya mwaka huu ya Kombe la Europa, kwa ushindi jumla wa mabao 4-2

Kikosi cha Leverkusen kinachonolewa na mkufunzi Xabi Alonso, kilikuwa katika hatari ya kupata kipigo chao cha kwanza tangu mwisho wa msimu uliopita, baada ya Leandro Paredes kutia kambani mabao mawili kwa njia ya penalti katika dakika ya 43 na 66 ya mchezo.

Hata hivyo, juhudi zao zilizaa matunda baada ya kupata bao la kujifunga kutoka kwa Gianluca Mancini katika dakika ya 82, kabla ya Josip Stanišić kulinda rekodi ya Leverkusen kwa kusawazisha bao la pili katika dakika ya saba ya muda wa ziada.

Sare hiyo ya Leverkusen iliivunja rekodi ya Benfica ya kutopoteza katika mechi 48, ambayo ilikuwa imeandikishwa kati ya mwaka 1963 na 1965. Leverkusen, ambao pia walitwaa taji la ligi ya Bundesliga, sasa ni kilabu pekee ambayo haijapoteza mchuano wowote barani Ulaya, na huenda wakatwaa mataji matatu msimu huu.

Mkufunzi Xabi Alonso ambaye aliahidi kuendelea kuwahudumia Leverkusen, anatarajiwa kuwaongoza kwenye fainali ya Kombe la Europa dhidi ya Atalanta tarehe 22 mwezi huu, pamoja na fainali ya Kombe la DFP Pokal tarehe 25 mwezi huu. Aidha, kikosi hicho bado kina majukumu ya mechi  mbili za ligi kuu dhidi ya Bochum na Augsburg.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *