Mkufunzi Paul Bitok, aliyekuwa mkufunzi wa zamani wa kikosi cha Malkia Strikers, amejiuzulu kutoka wadhifa wake kama naibu wa mkufunzi wa timu hiyo, siku kadhaa baada ya uteuzi wake mpya kuelekea michuano ya Olimpiki. Hatua hii imefuatia shutuma kutoka kwa wanamichezo na wadau wa mchezo huo nchini, baada ya wakuu wa shirikisho la KVF kujiteua kwenye nafasi za usimamizi.
Bitok, ambaye ni naibu rais wa Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF), ametangaza pia kujiondoa kutoka kwa majukumu ya kiufundi katika kikosi cha Malkia Strikers ili aweze kujikita zaidi katika majukumu yake ya kiutawala ndani ya KVF. Tangazo hili limetolewa mapema leo, kufuatia mvutano na malalamiko yaliyotokea baada ya uteuzi wa viongozi wapya wa shirikisho hilo kusimamia kikosi cha Kenya katika mashindano ya Olimpiki baadaye mwaka huu nchini Ufaransa.
Paul Bitok, aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, pia aliwahi kuwa mkufunzi mkuu wa Malkia Strikers na aliwaongoza kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2020. Katika kipindi cha uongozi wake, aliisaidia timu hiyo kushinda taji la African Games mwaka 2019 na taji la Africa Nations Cup mwaka 2023.
Kabla ya kujiuzulu, Bitok alikuwa ameteuliwa kusaidiana na Japheth Munala katika kuinoa Malkia Strikers, huku rais wa KVF, Charles Nyaberi, akipewa majukumu ya kuwa Meneja wa Timu (TM) wa kikosi hicho.