Jose Mourinho anakaribia kurejea kwenye ulingo wa ukufunzi baada ya kukubali masharti ya kuwa kocha mkuu wa klabu ya Fenerbahce. Mourinho, ambaye hajakuwa na timu tangu atimuliwe na Roma mwezi Januari, anatarajiwa kuchukua nafasi ya kocha wa sasa wa Fenerbahce, Ismail Kartal katika Ligi Kuu ya Uturuki, Süper Lig.
Mreno huyo anayejivunia ufanisi mkubwa barani Ulaya kwa kuongoza vilabu kama Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, na Manchester United, aliwaongoza Roma kutwaa taji la Europa Conference League msimu wa 2021-22. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Roma kushinda taji la Ulaya. Hata hivyo, alifutwa kazi kufuatia msururu wa matokeo duni kwenye kilabu hiyo.
Kocha wa sasa wa Fenerbahce, Ismail Kartal, anatarajiwa kuondoka kilabuni humo, huku kukiwa na fununu za uhusiano mbaya na usimamizi wa klabu hiyo. Iwapo atafaulu kutwaa mikoba ya ukufunzi, Mourinho ataungana tena na wachezaji wake wa zamani kama vile Fred, Edin Dzeko, Dusan Tadic, na Michy Batshuayi.