Kocha wa zamani wa Chelsea na Bayern Munich, Thomas Tuchel, ametangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza. Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) limetangaza kwamba Tuchel, mwenye umri wa miaka 51, amesaini mkataba wa miezi 18 na ataanza majukumu yake rasmi Januari 1, 2025. Mjerumani huyo anachukua nafasi ya Gareth Southgate, aliyeongoza timu hiyo katika mashindano ya Euro 2024 kabla ya kuachia ngazi.
Tuchel, ambaye aliwahi kuiongoza Chelsea kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021, ameeleza furaha yake ya kupewa fursa ya kuongoza timu ya taifa ya Uingereza na ameahidi kuleta mafanikio. Uteuzi wa Tuchel unamfanya kuwa kocha wa tatu wa kigeni kuiongoza Uingereza, akifuata nyayo za Fabio Capello na Sven-Göran Eriksson.
📩 (1) new message from Thomas Tuchel. pic.twitter.com/ADTVUHpnRN
— England (@England) October 16, 2024
Kocha huyo mpya wa Uingereza, atasaidiwa na kocha Muingereza Anthony Barry, ambaye aliwahi kufanya kazi naye katika vilabu vya Chelsea na Bayern Munich.
Kwa upande mwingine, Lee Carsley, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Uingereza ya vijana wa chini ya miaka 21, atasalia kuwa kocha wa muda wa Uingereza wakati wa mapumziko ya kimataifa ya Novemba. Carsley ataongoza timu hiyo katika mechi dhidi ya Ugiriki na Jamhuri ya Ireland kabla ya kurejea kwenye wadhifa wake.