Katika taarifa iliyotolewa kupitia tovuti rasmi ya Chelsea, usimamizi wa klabu hiyo umetangaza kuafikia makubaliano ya kuachana na Mauricio Pochettino kama mkufunzi mkuu. Hatua hii imekujia kwa mshangao kwa mashabiki wa kilabu ya chelsea, baada ya Pochettino kuhudumu kwa msimu mmoja pekee katika klabu hiyo.
Pochettino, mwenye umri wa miaka 52, aliteuliwa kuwa mkufunzi mkuu wa Chelsea mnamo Mei mwaka jana, akichukua nafasi ya Frank Lampard aliyekuwa kwenye wadhifa huo kikaimu. Katika kipindi chake cha ukufunzi, ameiongoza Chelsea kumaliza Ligi Kuu ya Uingereza katika nafasi ya 6, baada ya klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya 12 msimu uliopita.
Wakurugenzi wa Michezo kwenye kilabu ya Chelsea Laurence Stewart na Paul Winstanley walisema: “Kwa niaba ya kila mtu Chelsea, tungependa kutoa shukrani zetu kwa Mauricio kwa huduma yake msimu huu. Atakaribishwa tena Stamford Bridge wakati wowote na tunamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye ya ukufunzi.”
Wakufunzi wengine Jesus Perez, Miguel d’Agostino, Toni Jimenez na Sebastiano Pochettino pia wameondoka kwenye kilabu hiyo.
Chelsea sasa inatarajiwa kumteua mkufunzi mpya kabla ya msimu ujao kuanza. Mchakato wa kutafuta mrithi wa Pochettino unaendelea, huku mashabiki wa The Blues wakiwa na matumaini ya kuona mafanikio zaidi katika msimu ujao.