Stefano Pioli Kuondoka AC Milan Mwishoni mwa Msimu Huu

Pioli AC Milan

Mkufunzi wa klabu ya AC Milan, Stefano Pioli, ataondoka kutoka kwa wadhifa wake mwishoni mwa msimu huu. Pioli atakamilisha safari yake ya miaka 5 na klabu hiyo atakapoiongoza AC Milan katika mpambano wao wa mwisho kwenye ligi dhidi ya Salernitana siku ya Jumamosi.

Pioli, ambaye amekuwa akisuasua katika kuwinda mataji msimu huu, ataondoka baada ya mechi ya kesho huku kilabu hiyo ikiwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, alama 19 nyuma ya mahasimu wao Inter Milan. Licha ya changamoto za msimu huu, Pioli ataondoka na heshima na mapenzi ya mashabiki wa Milan baada ya kuwasaidia kushinda taji lao la kwanza la Serie A mwaka 2022, baada ya ukame wa miaka 11. Aidha, aliwawezesha kurejea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Mkataba wa Pioli ulikuwa unamalizika mwaka 2025, lakini pande zote mbili zimekubali kusitisha mkataba wake sasa. Kupitia mitandao yao rasmi, AC Milan imetoa shukrani zake kwa Pioli kwa mchango wake mkubwa katika klabu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *