Pamzo Atatuletea Taabu, Mkufunzi wa Kogalo Asema Kabla ya Mchuano wao.

Mkufunzi wa kilabu ya Gor Mahia, Jonathan McKinstry, anaamini kwamba kilabu ya Shabana itawapa wakati mgumu wakati watakapokutana katika mpambano wa ligi kuu siku ya Jumamosi. McKinstry ameeleza kuwa kocha wa Shabana, Sammy “Pamzo” Omollo, anaifahamu vyema Gor Mahia na huenda akawaletea changamoto katika mchezo huo utakaochezwa mjini Kisumu.

“Kocha Pamzo anaijua vyema K’Ogalo kwa kuwa alikuwa mchezaji wa klabu hii na pia yeye ni kocha mwenye mafanikio makubwa. Anaelewa fiziolojia ya Gor Mahia kwa kiwango fulani hivyo atakuwa na motisha ya kibinafsi sio tu kusaidia timu yake ya sasa lakini ni wazi, unapocheza dhidi ya timu yako ya zamani unataka kudhibitisha jambo,” alisema McKinstry.

Sammy Omollo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Gor Mahia, amewaongoza Shabana kushinda katika mechi tatu kati ya nne zilizopita, katika juhudi za kujiepusha na kushushwa ngazi na kurejea kwenye ligi ya NSL walikotoka msimu jana.

Shabana kwa sasa hivi wako katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali la ligi kuu, wakiwa alama mbili kutoka eneo la kushushwa ngazi, na wana imani kwamba wataweza kubadilisha matokeo na kuepuka kushushwa ngazi kwa kupata ushindi katika mechi zao tatu zijazo.

Mpambano kati ya Gor Mahia na Shabana utafanyika katika Uwanja wa Mamboleo mjini Kisumu Jumamosi saa tisa kamili adhuhuri, na utapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *